Alhamisi 9 Oktoba 2025 - 14:12
Hakuna nguvu ya kibeberu yenye haki ya kuamua hatima ya Palestina

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, katika ujumbe wake amesisitiza kuwa damu ya mashahidi wa Palestina imeuamsha dhamiri ya dunia na kuzielekeza fikra za umma kwenye haki za watu wanyonge wa ardhi hiyo. Amesema kuwa mustakabali wa Palestina utaamuliwa tu kwa mujibu wa matakwa na maamuzi ya Wapalestina wenyewe, na hakuna nguvu yoyote ya kibeberu au ya kigeni inayostahili kuingilia hatima ya taifa hilo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan, katika ujumbe wake huku akiashiria kuendelea uhalifu wa utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina amesema: “Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, utawala wa kigaidi wa Kizayuni wa Israeli umewammiminia wananchi wanyonge wa Palestina, hususan Ukanda wa Ghaza, milima ya dhulma na jinai — dhulma ambayo hakuna mfano wake katika historia ya hivi karibuni.”

Aliendelea kusisitiza kwamba: “Damu safi ya mashahidi wa Palestina na kusimama kwao imara leo kumezaa matunda. Hizi ndizo damu zilizomwagwa kwa dhulma ambazo sauti yake imetanda duniani kote, na mataifa huru, bila kujali rangi, kabila, dini au utaifa, yamepata msukumo kutoka kwenye roho ya mapambano na mshikamano na kusimama bega kwa bega na watu wa Palestina, wakati mwingine kupitia maandamano ya mamilioni ya watu na wakati mwingine kupitia harakati za wananchi kama vile "Flotila ya Ulimwengu ya Sumud"

Mwanazuoni huyu mashuhuri wa Pakistani, kwa huku akiashiria tamko la Trump kuhusiana Palestina, amelitaja kuwa ni mwendelezo wa wazi wa Tamko la Balfour. Amesema: “Ubeberu wa kimataifa umeilea na kuikuza ile mbegu ya umwagaji damu waliyopanda karne moja iliyopita hadi kuwa mti wa dhulma na ugaidi. Miaka mia moja imepita tangu tamko hilo la aibu, lakini wananchi wanyonge wa Palestina bado wanaendelea kupigania kupata haki zao za kibinadamu, kisheria na kitaifa.”

Ameendelea kubainisha kuwa: “Leo damu ya mashahidi wa Ghaza imezaa matunda na kuamsha dhamiri ya dunia; mataifa yameanza kulipa kipaumbele zaidi kuliko wakati mwingine wowote suala la Palestina, na hata wananchi wa kawaida kwa njia mbalimbali wameonesha ghadhabu zao dhidi ya jinai zinazofanywa utawala wa Kizayuni na kudhihirisha mshikamano wao na watu wa Palestina.”

Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan amesisitiza pia: “Mustakabali wa Palestina hautaamuliwa na nguvu yoyote ya kigeni; ni Wapalestina pekee ambao kupitia taasisi na vyombo vyao vya uwakilishi wataamua hatima ya ardhi yao. Katika Mashariki ya Kati hakuna dola ya kihistoria isipokuwa Palestina, na haitakuwepo nyingine; kwani wavamizi kamwe hawakuwa wenyeji wa ardhi hio. Wamiliki na warithi halisi wa ardhi hio ni Wapalestina pekee.”

Kwa kuashiria historia ya uvamizi wa Palestina ameongeza: “Zaidi ya karne moja sasa, ardhi hii imekuwa mhanga wa njama, mikataba na matamko ya kughushi ya nguvu za kibeberu. Mwanzo wa mchakato huu unarejea katika Tamko la Balfour mwaka 1917, wakati Arthur James Balfour, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza kwa wakati huo, alipoitoa hati hiyo iliyoweka msingi wa mradi wa Kizayuni. Mchakato huu ulifikia kilele mwaka 1948 kwa kuundwa utawala bandia na wa kigaidi wa Israeli, na kisha kuendelezwa kupitia mikataba ya kinafiki mbalimbali hadi ‘Makubaliano ya Ibrahimu’ na hatimaye ‘Tamko la Trump’ — yote yakiwa ni mwendelezo wa njia na kiini cha Tamko la Balfour.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Naqvi, mwishoni mwa ujumbe wake, huku akitoa heshima kwa mashahidi wa njia ya uhuru wa Palestina na kuonesha mshikamano na familia za waliopoteza makazi na waathirika wa vita vya Ghaza amesema:
“Bado tutaendelea kusimama pamoja na watu wa Palestina na katika mapambano haya ya kudai haki zao za kisheria, kibinadamu na kitaifa, tutaendeleza kuiunga mkono kimaadili, kisiasa na kidiplomasia.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha